Wanawake mnanisikia au niongeze sauti
WATAALAM wa saikolojia na elimu ya uhusiano wa kimapenzi kati ya mwanamke na mwanaume, tunakubaliana kwa pamoja kwamba, wanaume ni viumbe rahisi mno kuridhishwa kwenye suala la unyumba au tendo la ndoa. Mwanzoni, kitu kinachomhamasisha mwanaume ni muonekano wako tu wa kimahaba (kwa mwanamke). Lakini kadiri siku zinavyosonga mbele kwenye uhusiano, inakuwa ngumu kupandisha munkari wake, hata kama wewe ni mwanamke mrembo kiasi gani. Kumridhisha mwanaume wako inaweza ikawa rahisi kama tu utakumbuka kuweka mambo katika hali ya mvuto (remember to keep things interesting).
Tafuta namna ya kuleta hamasa kama ile iliyokuwepo siku za mwanzomwanzo wa penzi lenu. Kwa uhakika utakamata usukani. Pamoja na kumheshimu, kama mtazingatia sheria zifuatazo kwa makini, basi mwanamke hatakuwa na shida ya kumridhisha mumeo.
VAA VIZURI
Utamu wa faragha unaweza ukawa kwenye tendo lenyewe, lakini matamanio ya kufanya tendo hilo, yanategemeana na mambo mengine mengi. Vaa vizuri wakati wa kulala, wakati wote na siyo tu wakati wa usiku, ambao unataka kufanya tendo. Vaa nguo nyororo, yenye mtelezo unaomwagika mwilini. Kwa vazi hili na mtembeo wa kimahaba chumbani, mwanaume wako hatataka kutoa mikono yake mwilini mwako. Siyo unavaa vizuri tu ukiwa unakwenda sokoni na kwenye ibada, lakini nyumbani unajisahau
AIBU TUPA KULE
Usiwe mtu wa aibuaibu linapokuja suala la tendo. Mwanaume anaweza akakupenda kwa mapozi yako na aibu kwanza (lugha iliyotumika hapa ni ‘innocence’), lakini hakuna mwanaume atakayeendelea kuvumilia mwanamke ambaye anashtushwa kirahisi na kila kitu (mitindo ya tendo).
Wanaume wanapenda wanawake, ambao ni wataalam kwenye faragha. Wanaume wanapenda wanawake, ambao wana manjonjo mbalimbali wakati wa shughuli. Kama unataka kumridhisha mwanaume wako, basi soma mbinu ambazo zinatumiwa na wapenzi mbalimbali. Siyo akikuambia fanya hivi, unaanza eti hizo staili za kwa wanawake wako usiniletee, akikuambia fanya hivi, eti sitaki, kwanza niache nmechoka! Mwanaume hatakujibu kwa maneno, bali vitendo.
FANYA MAZOEZI
Wanaume ni watu wa kujali sana mwonekano wa mwanamke. Kwa hiyo siyo lazima kuonekana kama walimbwende, lakini mtazamo wa karibu na hapo, utakuongezea mvuto zaidi. Ndiyo, mwanaume wako anakupenda kama ulivyo, lakini lazima tuukabili ukweli kwamba watu wenye kufanya mazoezi wanaonekana na mvuto zaidi, hakuna kupinga hilo.
Hakikisha shughuli yako siyo ya kitoto unapokuwa kwenye kumi na nane. Siyo dakika mbili tu unahema kiasi kwamba unashindwa hadi kuendesha farasi.
KUWA MCHOKOZI
Hapa haimaanishi ule uchokozi wa kuleta ugomvi la hasha! Bali ni ule uchokozi, ambao kwa lugha ya Kiingereza unafahamika kama ‘tease’ kwa maana hiyo, basi tunasema ‘tease him’. Cheza naye michezo mbalimbali na uburudike naye ipasavyo. Kumbuka michezo isiwe ya kitandani tu, kama karata na kadhalika, bali michezo ya hata nje ya kitanda kama kukimbia na kucheza kidali po! Kama unataka kuwa mjuzi kwenye faragha, basi unatakiwa umfanye mwanaume wako akutake wakati wote na popote.
Tendo la ndoa siyo swichi ambayo unawasha na kuzima mnapokuwa chumbani tu. Mchokozechokoze hata kama mkisakata muziki chumbani. Mchokoze katika mitindo ya kimahaba bila kuvuka mipaka. Hata kama mmekwenda kwenye matembezi na kuchanganyikana na marafiki zenu, mkonyeze, mtege, usiogope kumpapasa, ringaringa na kujidekeza.
JIAMINI NA JIPENDE
Ndiyo, utaonekana vizuri zaidi ukipunguza unene, lakini hiyo haimaanishi kwamba haupo bomba. Hakuna kinachokera wanaume, kama mwanamke ambaye anauonea aibu mwili wake mwenyewe anapokuwa faragha. Jiamini kuhusu mwili wako na jaribu mambo mbalimbali na mwanaume wako. Mmenielewa au niongeze sauti?
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine tamu!
Comments
Post a Comment