Silaha 5 za mwanamke kumteka mwanaume kimapenzi
KATIKA maisha ya mapenzi watu wanapaswa kuelewana na kusikilizana mno. Hii ndiyo silaha kubwa zaidi kuliko zote na rahisi zaidi ya kukaa pamoja kwa muda mrefu. Pia mkisikilizana itasaidia wawili mnaopenda kudumu kwenye ndoa u uhusiano wenu hadi uzeeni.
Ikitokea mwanamke akamsikiliza vizuri mwanaume wake na mwanaume naye akamsikiliza vizuri mwanamke wake, basi mapenzi ya watu hawa yanaweza kuwa mfano kwa watu wengine watakaotamani kuwa kama wao.
Miongoni mwa vitu ambavyo watu wengi tunakosea kwenye mapenzi ni kujipa thamani na kujijali wenyewe zaidi kuliko wenzi wetu. Ni kosa kubwa! Jitahidi kumthamini mwenzio na huo ndiyo upendo wa dhati ambao hata Mwenyezi Mungu ametuagiza.
Hata hivyo, wanawake wengi wamekuwa wakikosea baadhi ya vitu kwenye kumpata mwanaume na kudumu naye. Inawezekana imetokea hivyo kwa kujua au kutokuja kabisa, anajikuta tu uhusiano wake umekatika ghafla.
Kwenye makala hii, leo nitawapa silaha tano ambazo mwanamke yeyote akiwa nazo atampata na kumteka mwanaume kimapenzi;
SILAHA YA KWANZA
Silaha ya kwanza anayopaswa kuwa nayo mwanamke ni kuwa na maisha yake na siyo maisha ya kuiga.
Wapo wanawake ambao hupenda kuiga kile kinachofanywa na wanawake wenzake na kudhani hivyo ndivyo anavyopaswa kuwa. Mwanamke mwenye tabia hii anaonekana ni mtu feki. Mwenye tabia hii huwa hana mvuto kwa mwanaume kwani atakuwa ni mwanamke feki. Ukweli ni kwamba wanaume wanapenda mwanamke anayeishi maisha halisi.
SILAHA YA PILI
Mwanamke anapaswa kuwa mtiifu na mwenye heshima na busara. Mwanamke hapaswi kuwa na kiburi na kutaka kuota mapembe kwenye uhusiano wake. Heshima na utiifu haimaanishi kuwa tayari kunyanyaswa, hapana. Mwanamke anapaswa ampe mpenzi wake au mumewe heshima inayotakiwa kama kichwa cha uhusiano wenu. Linapotokea jambo la kubishana kati yenu hasa mnapokuwa na watu wengine, mwanamke unapaswa kuzungumza kwa hekima na busara. Hii itamfanya mwanaume kuona mwanamke wake ni ‘kichwa’.
SILAHA YA TATU
Mwanamke anapaswa kuwa na uwezo wa kujitegemea. Hapa pana utata kidogo. Wapo wale wanaoamini kuwa mwanamke anapaswa kumtegemea mwanaume kwa kila kitu. Lakini ukweli ni kwamba wanaume wengi wanapenda kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye anaweza kusimama kwa miguu yake na kujitegemea pia.
SILAHA YA NNE
Mwanamke lazima awe anajiamini. Naam, hapa haimaanishi kuwa anatakiwa kuwa kiburi na mbishi, hapana. Isipokuwa mwanamke anapaswa aoneshe kujiamini kwa kile anachokisema na anachotenda. Lazima matendo yake yafanane na maneno yake. Asiwe na maneno mengi halafu vitendo ni sifuri.
Kujiamini kwa mwanamke kunamfanya mwanaume ajue kuwa ana mpenzi au mke ambaye anaweza kukabiliana na mikwaruzo mbalimbali inayohitaji hoja na utetezi.
SILAHA YA TANO
Mwisho, silaha nyingine ni kuwa na mvuto wa kipekee. Hapa haimaanishi kuwa mrembo sana, hapana. Ina maana kuwa mwanamke anapaswa kuwa nadhifu kila wakati ili kumfanya mwanaume apende kuwa nawe na avutiwe kuwa na wewe wakati wote.
Silaha hizi tano akiwa nazo mwanamke yeyote, basi mwanaume haruki na atambue fika kuwa mwanaume atavutiwa nawe na uhusiano wenu unaweza kudumu na kudumu na kudumu.
Silaha hizi zinaweza kukusaidia kumpata na kumteka mwanaume kirahisi kwani ndivyo vitu wanavyovihitaji. Kazi ni kwako wewe ambaye unatafuta mwenza wa kudumu naye maishani mwako. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua!
Comments
Post a Comment