CHAJIRANI KIHESHIMU
Juzi nilifuatwa na mwari wangu mmoja huku akilia, eti ohh mwanamke wa nyumba ya jirani amemchukulia mumewe. Shoga hivi utampaje nafasi mzee aende pembeni kujilinia asali bila hofu na mwisho kumiliki mzinga mzima? Kwa vile naheshimu ndoa, leo nataka nikung’ate sikio, sababu za nyumba ndogo kuwazidi kete wenye ndoa.
Najua siri hii itawachukiza wengi hasa wenye tabia ya kukwapua mali za watu na kujimilikisha waume hao kama wa kwao, tena wako radhi kuona familia za wenzao zikiteketea huku wao wakipata neema kutokana na kuchuna bila huruma. Kabla sijawapa siri za hao vishankupe wanaopenda kuchukua waume za watu kiasi cha kutuona siye tulioolewa si mali kitu, kwanza nataka niwaulize wale walioolewa maswali haya na kila mmoja ajibu kwa nafsi yake;
Nani anayefanya usafi wa mwili wa mume wako, kama vile kumkata kucha, kumnyoa nywele za pembe ya chaki na mambo mengine? Nani anayemfanyia masaji mume wako? Maana nawaona wengine macho yamewatoka pima kwa swali hilo la masaji, wengi hawajui kama mume anatakiwa kufanyiwa masaji, shuuuutuuuu! Basi huu ndiyo udhaifu unaozifanya nyumba ndogo kupata nguvu na kuwatawala waume zenu.
Sasa hujui lolote kati ya hayo niliyoyaeleza hapo juu, utaweza kumtuliza mumeo ndani? Siku zote adui hawezi kukushinda kama hajui udhaifu wako, mbaya zaidi udhaifu wako anaujua pale anapokutana na mumeo. Akimwangalia mumeo vidoleni anakutana na kucha zimechomoza kama kunguru la Pemba, kiwanja chake nywele zimemjaa kila kona, atashangaa, atamtia kwenye kumi na nane zake na wewe unakuwa ndiyo basi tena. Chefuuuuu!
Mzee ananogewa kwa majambozi, anakatwa kucha huku akikandwa na kupakwa mafuta, anasafishwa hadi kwenye kibendera cha kona, una nini tena mwari wangu wewe? Mali zako zinashikwa wakati wewe mwenyewe hujui hata ramani yake ikoje, niambie ni lini uliipiga deki ikulu ya mumeo?
Mwizi wako anapigilia msumari wa mwisho na kumzibua masikio mumeo, kisha mwanaume anagundua tofauti yako na ile ya nyumba ya pembeni, ikifikia hatua hiyo ujue umekwisha! Unashangaa mzee anakuwa na hasira hata kwa jambo dogo tu, hataki kula chakula chako na akirudi hata kukugusa hahitaji, upo nyonyo?
Haya ni kati ya makosa mengi ambayo wanawake walioko ndani ya ndoa wanayafanya, wengine wanayafanya bila ya kujua na wengine hawayajui kabisa na hawajui kama hawajui, eti wanalingia shepu zao, shepu peleka huko kijijini kwenu! Mwari wangu utaendelea kusimangwa kutokana na udhaifu wako, unaitwa mchafu kwa kuwa mumeo hajasafishwa, kila kona amejaa manyoya kama kondoo aliyetoroka machinjioni, hee eheeeiyaaaa!
Haya yote yanatokana na kufanya mambo kwa mazoea, kisha unalia kumbe matatizo umeyasababisha mwenyewe. Tuache tabia za kuwasubiri uwanjani, tunatakiwa kuwasubiri waume zetu wakitoka kazini ili tuingie nao bafuni kwa ajili ya kuoga pamoja.
Huko ndiko tutajua kama ikulu zao zina majani au la, huko ndiko tutaanzisha kampeni ya kulima mashamba yao na kukata nyasi na magugu yote.
Comments
Post a Comment