UKIKOSA SABABU; USIVUMILIE KWENYE MAPENZI
NIMEWASIKIA washauri wengi wakisema uvumilivu ni kitu muhimu katika mapenzi! Bila shaka hata wewe umewahi kuambiwa na wazazi au rafiki zako “vumilia tu” ukiaminishwa kuwa ndoa au mapenzi yana changamoto nyingi zinazohitaji uvumilivu.Kama hujui, uvumilivu ni mzigo mzito; ukikubali kuvumilia, lazima uwe na sababu ya kufanya hivyo.
Ukikosa sababu ya kuvumilia katika mapenzi hutakuwa tofauti na mtu aliyebeba furushi zito kichwani halafu hajui alipeleke wapi na wakati gani atalitua na kwa faida gani. Kamusi ya Kiswahili inaeleza maana ya uvumilivu kuwa ni; “Hali ya kustahimili machungu.” Huku kamusi hiyohiyo ikitafsiri ‘machungu’ kama matatizo makubwa yanayosababisha masikitiko.
Ukiambiwa vumilia maana yake uwe tayari kustahimili matatizo makubwa yatakayoleta masikitiko ndani ya moyo. Kwa kisingizio hiki kuna baadhi ya wanawake wanakesha wanalia kwa manyanyaso yasiyokoma kutoka kwa wapenzi wao. Ukiwauliza kwa nini hawaachani na matatizo hayo makubwa watakuambia; “Tunavumilia.”
Lakini uvumilivu wenye matumaini ndiyo wenye faida katika mapenzi na maisha kwa jumla, tofauti na hapo uvumilivu usiokuwa na matumaini ni mateso yanayoweza kuua. Watu wengi wamekufa katika ndoa kwa sababu waliishi kwa uvumilivu usiokuwa na matumaini; matokeo yake wakawa wanadhoofu afya ya mwili na akili na hatimaye kupoteza maisha.
Kumbuka unapovumilia machungu ya sindano kinachokutuliza ni matumaini ya kupata dawa ambayo baadaye itakuponya ugonjwa wako. Sababu chanya ndizo huwafanya wabeba mizigo mizito wavumilie kwani wanajua baadaye watapata fedha, wakulima watavumilia shida wakiamini mavuno yanakuja.
Utavumilia kazi na kitu chochote endapo tu mwisho wa machungu hayo utakuwepo akilini mwako na matumaini ya faida yatakuwepo. Kwa maana hii mtu yeyote akikuambia uvumilie machungu na matatizo katika mapenzi, usikubali kabla hujajua faida ya uvumilivu wako.
Lazima ujue na uamini kuwa uvumilivu wako katika mapenzi utakupa faida baadaye katika maisha yako na uwe na uhakika kuwa machungu yako ipo siku yatakoma. Tofauti na hapo usithubutu kuvumilia, utakufa. Kwani usipojua mzigo mzito wa uvumilivu wako utautua lini ni mateso ambayo heri ukayaepuka mapema kabla hujafa.
Kumbuka uvumilivu una faida kama saba hivi ambazo ukiwa nazo zitakusaidia kuufanya uvumilivu wako usiwe wa machozi, bali uwe wa faraja iliyojaa matumai ni.
Uvumilivu wako lazima uwe wa kukuwezesha kufanya uamuzi sahihi, hii ni faida ya kwanza. Ya pili, ni kukufiksha kwenye malengo yako ya ma isha.
Tatu, uvumilivu lazima uwe wa kukufanya kuwa mtu mwema kwenye jamii. Nne, uvumilivu wenye maana ni ule utakaofikisha kwenye muda sahihi wa kujinasua kwenye machungu. Tano, uvumilivu ukuwezeshe kupata vitu sahihi katika maisha yako. Sita, uvumilivu uwe ni shule ya kukufundisha upande wa pili wa maisha ya mapenzi.
Mwisho; ukufikishe kuwa shuhuda mzuri ili pale utakapofikia malengo na mipango yako uwe sehemu ya watu wa kutolewa mfano wa uvumilivu. Nakushauri jambo jingine muhimu; acha kuvumilia kwa kutaka kuutosheleza mwili kwani mwili huohuo unaoutosheleza ndiyo unaodhoofika kwa machungu
Comments
Post a Comment