Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 10)

ILIPOISHIA WIKIENDA…
NILIPOSHUKA tu nikamuona mwenyekiti akichungulia mlangoni. Aliposikia gari linasimama nyumbani kwake akachungulia.
“Vipi afande?” Akaniuliza.
“Mlipoondoka nikakumbuka kwamba nilisahau kitu.”
“Kitu gani?”
“Nilisahau kumuonesha picha za watu wawili ambao tunawashuku. Huenda huyo aliyemuona akawa mmojawapo.”
“Sasa ameshakwenda nyumbani kwake.”
“Tafadhali nipeleke anakoishi.”
Ingawa hapakuwa mbali na nyumbani kwake, mwenyekiti huyo alinipeleka nyumbani kwa msichana huyo. Nyumba aliyokuwa anaishi ilikuwa ikitazamana na nyumba aliyokuwa akiishi Matilida.
SASA ENDELEA…
NILIVYOPIMA zile nyumba zilivyo, niligundua ni kweli ulikuwepo uwezekano wa Salma kumuona Matilida akishuka kutoka kwenye teksi. Hata hivyo, kwa vile ilikuwa usiku inakuwa ni vigumu kuigundua sura ya mtu. Pengine ndiyo sababu alishindwa kunitambua.
Mwenyekiti aliposhuka kwenye gari na mimi nikashuka. Mwenzangu alitangulia kufika mlangoni, akamuita Salma.
Mpaka mimi nafika kando ya mlango huo, Salma alikuwa ameshatoka nje.
“Salma nimekufuata tena. Nilikuwa na tatizo dogo,” nikamwambia Salma kabla hajauliza kulikoni.
“Tatizo gani afande?” Salma akauliza kwa sauti ya wasiwasi.
“Kuna picha mbili za watu ambao tunawatuhumu kuhusika na mauaji ya Matilida. Nilisahau kukuonesha picha hizo. Angalau ungeziona ungeweza kutueleza kama huyo mtu uliyemuona akishuka kwenye teksi na Matilida ni mmojawapo.”
Salma akanyamaza na kunitazama. Nikahisi kama vile aliona ingemuia vigumu kumtambua mtu huyo kwenye picha.
“Si ulisema ukimuona unaweza kumtambua?” Nikamuuliza.
“Ndiyo nikimuona nitamjua kwa sababu sura yake si ngeni kwangu.”
Aliporudia kusema hivyo niliuelekeza uso wangu upande mwingine ili asiuone vizuri.
“Sasa ukiziona picha hizo kama huyo uliyemuona ni mmojawapo utatuambia.”
“Sawa.”
“Sasa turudi kituoni mara moja utusaidie katika zoezi hili.”
“Sawa. Tunaweza kurudi.”
Iliwezekana kumuonesha picha hizo hapohapo kupitia kwenye simu yangu, lakini sikutaka kufanya hivyo. Kitendo hicho kilikuwa sawa na kujidanganya mwenyewe kwa sababu nilikuwa nikifahamu kwamba walioko katika picha hizo siyo walioshuka na Matilida kutoka kwenye teksi. Aliyeshuka na Matilida nilikuwa mimi.
Hivyo niliona kumuonesha picha hizo hapohapo huku nikijua kwamba hakukuwa na yeyote ambaye angemtambua, niliona ilikuwa sawa na kujidanganya mwenyewe.
Lengo langu lilikuwa kumdanganya Inspekta Mwakuchasa. Kwa hivyo niliona niende naye kituo cha polisi ili Mwakuchasa aone kuwa zoezi hilo limefanyika japokuwa nilijua msichana huyo asingemtambua yeyote kati ya watuhumiwa hao.
Nilipokubaliana na msichana huyo kwamba nirudi naye kituoni, nilimpakia kwenye gari na kwenda naye kituoni.
Tulipofika nilimwambia Inspekta Mwakuchasa.
“Nimekuja naye, ninakwenda kumuonesha zile picha.”
Mwakuchasa akatufuata. Tulikwenda kwenye ubao uliokuwa umepachikwa matangazo na picha mbalimbli za watuhumiwa.
Nilimuona mke wangu akipita nyuma yetu na kututazama. Laiti asingekuwepo Inspekta Mwakuchasa hapo, msichana huyo kutokana na wivu wake angekuja kusimama hapohapo akajifanya anatazama zile picha.
Lakini alipita na kwenda kaunta.
Nilimuonesha Salma picha hizo mbili za watuhumiwa hao ikiwemo picha ya Mdachi.
Salama alizitazama picha hizo kisha akatikisa kichwa.
“Hizi sura sizo kabisa,” alisema.
“Umeziangalia vizuri?” Mwakuchasa akamuuliza.
“Ndiyo. Nimezingalia viuri. Hapa hayupo.”
Mwakuchasa akanitazama.
“Huyo sasa atakuwa mtuhumiwa wetu wa tatu?” Akaniambia.
“Ndiyo afande.”
Mwakuchasa akamtazama Salma.
“Wewe humfahamu?”
“Mimi simfahamu, lakini sura yake si ngeni kwangu.”
“Huwa unamuona wapi?” Mwakuchasa aliendela kumuuliza.
“Namuona humuhumu mjini, sura yake si ngeni kwangu kabisa,” msichana alisema kisha akanitazama mimi mara moja kabla ya kuyarudisha macho yake kwenye zile picha.
Jinsi alivyonitazama na jinsi alivyopenda kuyarudia yale maneno yake kwamba sura yake si ngeni na anamuonaona humu mjini, vilifanya nijishuku kwamba huenda ananisema mimi. Huenda alishagundua kuwa aliyeniona ni mimi, lakini aliogopa kutamka hivyo.
“Sasa sikiliza. Ushirikiano wako ni muhimu kwetu. Wakati wowote utakapomuona mahali popote, tupigie simu haraka utuarifu,” Mwakuchanasa alimwambia msichana huyo kisha akanitazama mimi.
“Utampa namba yako ya simu.”
“Sawa afande.”
“Mrudishe.”
Mwakuchasa aliondoka na kurudi ofisini kwake na mimi nikaondoka na Salma. Nilipotoka tu nje ya kituo, mke wangu akanifuata.
“Unakwenda wapi?” Akaniuliza huku akimtazama yule msichana.
“Namrudisha huyu msichana nyumbani kwake.”
“Kwani alikuwa na tatizo gani?”
“Yule msichana aliyeuawa juzi, huyu anaishi jirani yake na pia ni rafiki yake. Amekuja kutupa maelezo.”
“Sasa pale mlikuwa mnatazama nini?”
“Anatazama zile picha za watuhumiwa tulizoziweka. Tulitaka atambue kama kuna mmojawapo anayemfahamu.”
“Sasa ndiyo unamrudisha nyumbani kwake?”
“Acha nimfikishe mara moja.”
Nilimtazama Salma, nikamwambia.
“Salma twende.”
Tukaenda kujipakia kwenye gari. Nilihisi kama mke wangu aliona uchungu sana, lakini ni mambo ya kikazi. Hata yeye akihudumia wanaume, mimi siwezi kuchukia.

Nikaliwasha gari na kuondoka.
Wivu mwingine hauna maana kabisa. Yule msichana sikuwa nikimtamani na wala sikuwa na nia ya kumtongoza. Adabu niliyoipata kwa Matilida imetosha.
Nilipomfikisha Salma nyumbani kwake, nikashtuka, nilipoliona gari la kifahari ambalo niliamini lilikuwa gari la Azzal Mabruki. Lilikuwa limeegeshwa nje ya nyumba ileile. Ndani halikuwa na mtu.
Wakati nimesimamisha gari mbele ya gari hilo, nilimuuliza Salma;

“Hili ni gari la nani?”
”Ni la jamaa mmoja…” Salama alinijibu, lakini nilihisi alikuwa amebakisha maneno.
Nilipomuona amefungua mlango ili ashuke nikahisi kwamba hakutaka tuendelee kuzungumza kuhusu mtu huyo.
“Hebu subiri,” nikamwambia.
Msichana akarudi kwenye siti.
“Huyu jamaa amemfuata nani hapa?”
“Kuna msichana wake humu ndani.”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Uaridi.”
“Anaitwa Uaridi?”
“Ndiyo.”
“Yuko naye muda mrefu?”
“Ndiyo yuko naye muda mrefu.”
“Baadaye nitakuwa na mazungumzo na wewe.”
“Saa ngapi?”
“Nipe namba yako nitakupigia usiku.”
Msichana alinipa namba yake.
“Yangu nilishakupa.”
“Ndiyo yako ninayo.”
“Basi wewe nenda, ni hapo nitakapokupigia.”

Msichana alifungua mlango na kushuka. Na mimi nikaliondoa gari. Kwa mbali nilihisi mwili wangu ukitetemeka. Kitendo cha kukuta gari la mtu niliyekuwa nikimshuku kuhusika na mauaji ya Matilda, mbele ya nyumba ya msichana aliyedai kwamba alimuona Matilida usiku akishuka na mwanaume kutoka kwenye teksi, kwa kweli kilinishtua sana.

Nilihisi mambo mengi. Nilihisi kwamba huyu msichana huenda anajua siri ya kuuawa kwa Matilida, lakini anaficha. Sikukumbuka kwamba usiku ule niliporudi na Matilida niliona gari hilo kwenye ile nyumba.

Lakini kama lilikuwepo basi ni Azzali Mabruki aliyemuua Matilida. Alituona wakati tunashuka kwenye teksi na akatambua kuwa nilikuwa ni mimi. Baadaye akaja kubisha mlango. Matilida alipomfungulia akampiga chupa ya kichwa na kuondoka.
Hili suala nisingeweza kulichunguza peke yangu. Ilinipasa nitengeze hoja ya kulifikisha kituoni ili Mabruki akamatwe.
Je, nini kiliendelea? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.






Comments

Popular posts from this blog

SHANGAZI NAE ANATAKA-07

join sugar mumy and dating whatsapp group link