Kutokwa uchafu sehemu za siri ni dalili za magonjwa haya
SEHEMU za siri za mwanamke, pamoja na mambo mengine huwa ni njia au kiunganishi baina ya sehemu ya nje za mwili na viungo vya uzazi vya ndani vya mwanamke. Majimaji yaliyo kwenye sehemu za siri za mwanamke huwa ni ya tindikali, hali inayosaidia kuzuia maambukizi ya vijidudu wanaoweza kuleta maradhi. Hali hii ya utindikali husababishwa na bakteria waishio katika eneo hilo la mwanamke. Hawa ni bakteria wa kawaida wasio na madhara yoyote kwenye mwili. Sehemu hizo za siri zinapokuwa katika hali nzuri, hutoa majimaji haya ili kujisafisha.
Majimaji haya ambayo pia hutengenezwa katika eneo la cervix hufanya kazi ya kuondoa seli zilizokufa pamoja na bakteria waharibifu nje ya mwili na huu ndio uchafu wa kawaida ambao mwanamke huutoa. Njia hii sehemu za siri za mwanamke hutoa bakteria wabaya na seli zilizokufa na kwamba ni njia ya kujisafisha na kuzuia maambukizi ya magonjwa.
Kitu chochote ambacho kitaharibu uwiano wa utengenezaji wa majimaji haya kinaweza kujenga mazingira ya maambukizi kuwa rahisi. Wanawake wote hutoa uchafu huo sehemu za siri. Kiwango cha uchafu unaotoka, rangi yake na harufu yake vitabadilika kutoka kipindi kimoja hadi kingine kulingana na muda mwanamke aliopo katika mzunguko wake wa mwezi.
Uchafu huu utabadilika vilevile kama mwanamke ananyonyesha, atakuwa na hisia za kufanya mapenzi, atakuwa na mabadiliko ya lishe, anatumia dawa hasa ya mpango wa uzazi au atakuwa na ujauzito. Kwa kawaida uchafu huu huwa hauna rangi na huwa wenye rangi yenye weupe wa mawingu au njanonjano pale unapokaukia kwenye nguo. Unaweza kuwa na vijipande vidogovidogo na mara nyingine ukawa wa kunatanata.
Kwa mujibu wa mtandao wa healthoniline, maambukizi katika sehemu za siri ni tatizo la kawaida kwa wanawake na kwamba wanawake wengi wameshapata tatizo hilo angalau mara moja katika maisha yao. Unasema mwanamke akiona yafuatayo, ajue anaweza kuwa na tatizo la maambukizi na hivyo ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya.
Mambo hayo ni pamoja na kutokwa uchafu sehemu za siri kunakoambatana na kuwashwa au vijipele, kutokwa na uchafu ambako ni endelevu na kwa kiwango kinachozidi hali ya kawaida kila siku au kusikia maumivu wakati wa kutoa haja ndogo. Mengine ya kuangalia, ni kutokwa na uchafu mweupe, mzito kama jibini au uchafu kuwa na rangi ya kijivu, mweupe, njano au kijani unaotoa harufu.
Kitu chochote kitakachoharibu uwiano wa bakteria wa kawaida waishio katika sehemu za siri za mwanamke, kinaweza kuleta mabadiliko katika rangi, harufu au muundo wa uchafu utakaotoka. Uchafu wenye damu na rangi ya kahawia ni dalili ya mzunguko wa mwezi wa mwanamke uliovurugika na mara chache inaweza kuwa dalili ya saratani ya kizazi.
Mwanamke mwenye tatizo hili huweza kutoa damu nyingi na kuumwa nyonga, mwanamke akitokwa na uchafu wenye rangi ya mawingu au njano hiyo ni dalili ya ugonjwa wa kisonono. Hapo mwanamke anaweza kutokwa na damu katikati ya siku zake, atatokwa na mkojo bila kukusudia na kupata maumivu ya nyonga.
Mwanamke akitokwa na uchafu wa rangi ya kijani unaoambatana na harufu na ikiwa uchafu utatoka kama mapovu, wenye rangi ya kijani au njano ukiambatana na harufu, inaweza kuwa ni dalili ya mambukizi yanayotokana na ngono zembe na kuambukizwa Trichomoniasis au parasitic.
Dalili nyigine inayomhitaji mwanamke kumwona daktari ni maumivu na kuwashwa wakati wa kutoa haja ndogo. Lakini ukitokwa na uchafu mweupe mzito kama maziwa ya mtindi, hiyo ni dalili ya maambukizi yatokanayo na fangasi (Yeast Infection). Dalili nyingine anazoweza kuzisikia mwanamke huyu ni kuvimba au kusikia maumivu sehemu za nje za siri (vulva). Anaweza kuwashwa au kusikia maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
USHAURI
Ukiona dalili hizo muone mtaalamu wa afya, atakupima na kukupa dawa husika kutokana na vipimo.
Comments
Post a Comment