‘I LOVE YOU’ NYINGI ZA NINI? UKIPENDA ONESHA MATENDO!
MAPENZI yanachukua nafasi kubwa katika maisha yetu. Mimi na wewe tunahitaji kuwa na wapenzi tena wenye mapenzi ya dhati ili maisha yawe ni yenye furaha na amani. Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo wanaochukulia mapenzi kama kitu rahisirahisi. Hapa namaanisha hivi, mtaani kuna watu wa aina mbili.
Kuna ambao wanajua kweli kupenda. Akisema anampenda fulani, anamaanisha na kuna wale ambao wanaweza kusema wamependa kumbe hamna lolote.Unamkuta mwanaume anadanganya kuwa ametokea kumpenda msichana fulani na ana dhamira ya kufunga naye ndoa lakini kumbe hana lolote, nia yake amuonje kisha aingie mitini.
Achilia mbali hao, kuna wanaume ambao wanatumia pesa na utaalam wao wa kuongea kuwarubuni wasichana ili watembee nao kwa kipindi fulani kisha wakisharidhika, wanawaacha. Wavulana hao wapo na wamekuwa ni tatizo kubwa huko mtaani.
Lakini pia wapo wasichana ambao wenyewe wanajiita wa mjini. Yaani wao hawajui kupenda, wanachoangalia ni mwanaume ‘mwenye nazo’. Wakishampata, watajifanyisha kuwa na mapenzi ya dhati kupita maelezo kumbe hamna kitu, usanii mtupu!
Katika mazingira hayo sasa utaona ni kwa jinsi gani mapenzi yamekuwa janga. Ndiyo maana leo hii wapo wanaotamani kutojihusisha na mambo ya mapenzi kwa sababu hizihizi za usanii na ujanjaujanja mwingi.Wakati mambo yakiwa hivyo, kuna baadhi ya watu ambao wamekithiri kwa tabia ya kuwatesa wapenzi wao kisa wameoneshwa kuwa wanapendwa sana.
Wapo watu ambao wakipenda wamependa kweli na hawawezi kujizuia kuonesha hisia zao kwamba ‘wamekufa’. Hatua hiyo sasa hivi badala ya kuwa changamoto kwa aliyependwa ili naye aongeze mapenzi, inakuwa tatizo.Uchunguzi umebaini kuwa, mwanaume akioneshwa kupendwa sana na mwanamke, atavimba kichwa na kumfanyia mwenzake kila aina ya visa eti kwa kuwa amebaini amezimikiwa. Hili halipo kwa wanaume tu. Wapo wanawake ambao nao kwa kujua kuwa waume zao ‘wamekufa’ kwao, dharau inaongezeka, heshima inapungua na kufanya hata yale ambayo wanajua yanawakera wenzao.
Hivi kwa nini tufikie hatua ya kuwaliza na kuwanyanyasa watu ambao wameshindwa kujizuia kuonesha mapenzi yao kwetu? Kama ulikuwa hujui basi leo tambua kuwa, anayekupenda kwa dhati kisha wewe ukamfanya kila siku ni wa kulia, chozi lake haliendi bure. Inaweza kuwa ni tatizo kwako na hata pale atakapoamua kunyoosha mikono juu, unaweza kushangaa unakutana na majanga kibao na kujutia uliyokuwa unayafanya.
Mimi nadhani kama humpendi mtu ni vyema ukamwambia mapema ili ajue kwamba, kama atatumia nguvu na muda wake mwingi kwako, ni kazi bure. Unapokubali kuwa na wewe unampenda kisha baadaye unaanza kumfanyia vioja, ni dhambi hata kwa Mungu.
Iko hivi, kama kweli unapenda, mdhihirishie kwa matendo ili asiwe na shaka kwamba huenda ameingia kwenye penzi la kisanii. Kama yeye amekutamkia kuwa anakupenda lakini wewe ukahisi huna mapenzi naye, kuwa muwazi kwake ili ajue wazi amempenda mtu ambaye hampendi!
Comments
Post a Comment