HATA UKIFANYIA GIZANI, DUNIA HAINA SIRI
NI siku nyingine nzuri tunapokutana kwenye ukurasa huu, mahali ambapo tunajadiliana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi na maisha kwa jumla. Tumewahi kujadiliana hapa kuhusu madhara ya usaliti katika mapenzi, kwa sababu maalum, leo nataka tujadiliane tena katika sura nyingine.
Ipo hivi, hakuna kosa kubwa katika uhusiano wa kimapenzi kama kumsaliti umpendaye. Vitabu vya dini zote vinaeleza wazi kwamba kosa pekee linaloweza kusababisha uhusiano wa kimapenzi ukavunjika, hata kama wawili watakuwa wamefunga ndoa kanisani au msikitini, ni USALITI!
Unapomkamata mwenzi wako amesaliti, sheria inakuruhusu kabisa kuachana na mwenzi wako, hata kama mtakuwa mmefika mbali kiasi gani katika maisha. Kinachoshangaza ni kwamba licha ya jambo hilo kuwa wazi kabisa, bado wanandoa wengi wanachepuka.
Upo ushahidi wa wanawake wenye heshima zao, wake za watu, ambao kwa sababu wanazozijua wao, wanawasaliti waume zao. Upo ushahidi pia wa wanaume wenye heshima zao, wengine wakiwa na pete zao vidoleni, wanawasaliti wake zao.
Ukifuatilia wengi wanaosaliti, vichwani mwao huwa wanaamini kwamba wanachokifanya ni siri na hakuna anayeweza kuja kugundua! Nikukumbushe tu kwamba dunia haina siri na siku zote Mungu huwa hamfichi mnafiki!
Unamdanganya kwa maneno matamu kwamba wewe ni wake pekee, hakuna mwingine unayempenda zaidi yake na hakuna kitakachowatenganisha zaidi ya kifo! Lakini kumbe nyuma ya pazia, unatoka na mtu mwingine! Unaamini kwamba ni siri, hawezi kuja kugundua. UNAJIDANGANYA!
Kama kweli unaipenda ndoa yako, kama kweli unampenda mkeo au mumeo, jiwekee nadhiri ndani ya moyo wako kwamba hutamsaliti maisha yako yote! Hiyo ndiyo heshima ya ndoa, hiyo ndiyo heshima ya mume au mke na ninakuhakikishia inawezekana.
Unapopatwa na mawazo ya kushawishi, hebu jiulize, siku mwenzako akija kugundua itakuwaje? Usijidanganye kwamba hatakuja kugundua, atajua tu, hata kama siyo leo wala kesho, lakini ninakuhakikishia ipo siku atajua. Utakuwa na lipi la kumweleza? Upo tayari maisha mliyohangaika kuyajenga kwa miaka yote hiyo yakaishia hewani kwa sababu ya tamaa zako?
Upo tayari kumpoteza umpendaye kwa sababu ya mwanamke au mwanaume wa nje? Ukishapata majibu, basi unaweza kuendelea na unachokifikiria, lakini kama unaona haupo tayari, ni bora ukaepusha matatizo, mshinde ibilisi wa usaliti kwa sababu inawezekana.
Kabla ya kusaliti, jiulize kwa nini unataka kusaliti? Ni kwa sababu mwenzi wako haikati kiu yako muwapo faragha? Una uhakika gani kama huko unakoenda kuchepuka kiu yako itakatwa? Mbona zipo njia za kumfanya awe bora? Kwa nini usifikirie kumsaidia ili awe bora?
Je, unasaliti kwa sababu ya fedha? Unaamini fedha ina thamani kuliko utu wako? Watu wangapi wanazo fedha, lakini hawana furaha ya mioyo yao? Usijidanganye! Fedha huwa haimtoshi mtu na kamwe haiwezi kukuletea furaha, lakini mapenzi ya dhati yanaweza kukufanya ukawa na furaha hata kama huna fedha.
Ihangaikie furaha ya penzi lako, achana na tamaa za mambo ya kupita! Kubaki njia kuu kutakusaidia kuepusha matatizo makubwa yanayoweza kuikumba ndoa yako au uhusiano wako siku ukija kugundulika. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
Comments
Post a Comment