MAMBO YA KUFANYA MPENZI WAKO AKIKUFANYIA KISIRANI
KWA watu waliopo katika uhusiano wa kudumu, watakubaliana na mimi kwamba kuna wakati huwa inatokea mwenzi wako anaamua tu kukufanyia kisirani, na hii inawahusu zaidi wanawake, hataki kuzungumza chochote na wewe. Kila unachomuuliza anakujibu kwa mkato kisha anaendelea na mambo yake, hataki kushirikiana chochote na wewe na hata haki yako ya msingi huipati!
Wengine huweza kudumu kwenye hali hii kwa muda mrefu na kama usipokuwa makini, hii inaweza kuwa sababu itakayowaingiza kwenye matatizo makubwa zaidi. Bahati mbaya ni kwamba ni wanaume wachache sana wanaoelewa nini cha kufanya inapotokea mwanamke unayeishi naye, au unayempenda sana anakubadilikia kiasi hiki.
Yaani unamuona kabisa hayupo sawa, hakuchangamkii, hataki kuzungumza na wewe lakini unapomuuliza kama ana tatizo lolote, anakujibu kwamba hakuna tatizo lolote na yupo sawa. Wengine hudhani kwamba mwanamke husika ameanza dharau, amepata wanaume wanaompa jeuri au hampendi tena!
Kama nilivyosema, ukishindwa kujua hali yake imesababishwa na nini na unatakiwa kufanya nini ili kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida, unaweza kujikuta ukisababisha matatizo makubwa zaidi. Kwa hiyo, jambo la msingi unatakiwa kuwa
mwepesi kumsoma mwenzi wako na hii itakusaidia kumgundua muda ambao hayupo sawa.
Ukishagundua kama hayupo sawa na anakuwekea mgomo baridi, muulize kwa upole kama yupo sawa au kama kuna kitu kinamsumbua. Bila shaka majibu yake yatakuwa ni yaleyale, ‘nipo sawa’, ‘hakuna tatizo’ na mengine ya aina hiyo. Ukishamuuliza mara moja au mbili akakujibu vilevile, huna haja ya kuendelea kumuuliza mara nyingi zaidi kwani utasababisha azidi kukasirika.
Kwa jinsi tulivyoumbwa, wanawake wanaongozwa zaidi na hisia. Unapomuudhi mwanamke wako jambo fulani, kitu pekee anachoweza kukifanya kukuonesha kwamba amekasirika, ni kukulalamikia lakini akiona huelewi au kama humpi nafasi ya kulalamika, basi huishia kukununia. Kwa hiyo unapoona amefika katika hali kama hiyo, tambua kwamba kuna ujumbe anataka kukufikishia!
Anataka kukuonesha kwamba umemkasirisha, umemuumiza moyo wake na hafurahishwi na matendo yako. Unachotakiwa kufanya kwanza ni kutulia lakini pili ni kuanza kujichunguza mwenyewe, ni jambo gani umefanya mpaka ukamuudhi? Jiulize mwenyewe ndani ya kichwa chako lakini wakati huohuo, tambua kwamba anahitaji sana ‘attention’ yako.
Mwanamke akinuna, anataka umuoneshe kwamba umeshaelewa kwamba hayupo sawa na unajitahidi kumfanya arudi kuwa sawa! Wengine wanakosea kwamba akishaona amenuniwa, basi na yeye anaanza visa, anaanza kufokafoka na kuwa mkali, hayo ni makosa.
Unatakiwa kushuka chini hata kama bado hujajua kosa lako ni lipi, kuwa mpole kwake, muoneshe kumjali, jitahidi kujiweka karibu naye na mfanyie mambo mazuri. Kama unajiweza, unaweza hata kumuomba mtoke ‘out’, kama amekasirika sana anaweza hata kukataa kutoka na wewe lakini ni jukumu lako kumbembeleza.
Kihulka wanawake wameumbwa kubembelezwa kwa hiyo katika mazingira kama hayo ni nafasi yako ya kuonesha uwezo wako wa kumbembeleza mpaka akubaliane na kile unachokitaka. Ukishapata nafasi ya kutoka naye, au hata kama hamjatoka mpo wenyewe mahali tulivu, anza kuzungumza naye kwa upole ukitanguliza maneno matamu ya kujishusha na kumuomba akusamehe, bila shaka kama kuna jambo umemuudhi atakueleza kwa uwazi, hata kama unaona siyo jambo la msingi sana, rudia kumuomba radhi na mhakikishie kwamba halitajirudia.
Utashangaa anaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida na lile tabasamu lililopotea kwenye uso wake litaanza kuchanua upya. Ukitumia nguvu na ubabe, utakuwa sawa na mtu anayemwagia petroli kwenye moto. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
Comments
Post a Comment