JIHADHARI NA MAADUI WA PENZI LAKO
NI Ijumaa nyingine murua. Siyo mbaya kwa wanajamvi hili, ndugu, jamaa na marafiki kushirikiana katika mapenzi kama vile wakati wa sherehe au msiba.
Pia siyo mbaya kujuliana hali na kutambulishana mambo ya msingi yanayoendelea kwenye uhusiano wako na mpenzi wako.
Hata hivyo, kuna wakati watu wengine wa pembeni, wawe majirani, ndugu, wazazi au marafiki wanaweza kuwa sumu ya uhusiano wako, hasa pale unapowategemea sana kutoa msaada, maoni au maelekezo katika maisha yako ya kimapenzi. Kuna mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano wa rafiki, ndugu, jamaa au wazazi kuwa kuvuruga penzi lako.
Kwanza kabisa ni kujitahidi kudhibiti taarifa zenu kwenda kwa wengine; kadiri unavyoelezea uhusiano wako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi watu kutoa maoni na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako.
Katika eneo hili, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu masuala yako ya uhusiano kabla hujaanza kutafuta maoni na ushauri kwa wengine. Ni bora ukasoma vitabu, na mada mbalimbali, hususani zihusuzo tabia na maisha ya uhusiano, zitafakari vema ili kuona zinahusiana vipi na unayokumbana nayo katika mahusianao yako.
Pili ni lazima uwe na uwezo wa kufanya mambo yako kipekee; Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako. Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo katika uhusiano na kutafuta suluhisho kabla ya kutegemea watu wengine.
Tatu ni lazima ujue mwenye uamuzi ni wewe; ni kweli kwamba kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wengine na zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini, hakikisha kuwa unatambua kuwa wewe mwenyewe ndiye mwenye kubeba lawama ya uamuzi utakaochukua.
Nne ni lazima uwe na subira; Usichukue uamuzi wa haraka katika uhusiano hususan uamuzi wa kuamua kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo uhusiano wako. Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa haraka, unajinyima nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha, hususan madhara yanayoweza kutokea kwa kuwaeleza wengine au kama ni tatizo, basi kufikiria njia sahihi ambazo ungeweza kuzitumia kupata suluhu ya tatizo.
Tano ni kufungua njia za mawasiliano kati yenu; Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani yanayohusu uhusiano wenu kwa watu wengine ni kwa kuwa umekosa nafasi ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za kutosha, jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka kuwashirikisha wengine.
Sita ni vyema kuwa peke yenu; Hata kama hutaki kueleza watu kuhusu mambo yanayoendana na maisha yenu, mazingira unayoishi yanaweza kuchangia watu kutaka kuingilia uhusiano wenu kwa kutoa maelekezo, ushauri au maoni kuhusu muishivyo wewe na mpenzi wako. Inapobidi hakikisha hamuishi karibu na wazazi wenu, ndugu au rafiki wa karibu.
Au hufanyi kazi na mwenzi wako sehemu moja, kwani hiyo itakuwa njia rahisi sana ya watu kuona mnavyoishi. Inapobidi kuwa karibu na watu wengine, hakikisha mnakubaliana wewe na mwenza wako namna bora ya kuendesha mawasiliano kati yenu mbele za watu, ili msiwape nafasi ya wao kuanza kutoa maelekezo ya vile wanavyoona mnapaswa kuishi.
Comments
Post a Comment