UNAIKUMBUKA AHADI YAKO WAKATI UNAANZISHA UHUSIANO?-2

MARAFIKI hili ni somo muhimu sana kwa wapendanao, kujua ahadi ambazo zinaweza kuwa na nakshi katika mapenzi na zile ambazo huleta migogoro. Tulianza kwa uchache wiki iliyopita, hebu sasa twende tukaone ahadi mbalimbali zinazotolewa na wenzi wengi wa siku ambazo mara nyingi huleta madhara.

MAMBO SAFI!

Baadhi ya wanaume wanakutana na wenzi wao kwa mara ya kwanza, ili wasidharaulike huanza kujisifu kwamba wanatoka katika familia zenye uwezo. Kwa kutumia njia hii, huwa na imani kwamba watakubaliwa kwa urahisi zaidi kwa vile wanatoka katika familia zenye uwezo mkubwa kifedha. Hili ni tatizo katika siku za mwanzo wa uhusiano, kwanza kwa mwanamke mwenye akili, atakudharau badala ya kukupa heshima. Atakuona wewe ni mwanaume tegemezi ambaye unajisifu kwa sababu ya mali za familia.

Hata hivyo, hii si sifa kubwa ambayo itamfanya mwanamke (mwenye uelewa) akukubali, kwa sababu unaonekana una majigambo. Mwanaume thabiti hazungumzii juu ya familia yake. Mtu wa aina hii humuahidi mpenzi wake kumsaidia kwa kuwa anatoka katika familia yenye hali nzuri kifedha. Huu ni ushawishi wa kizamani sana.

Hata hivyo, utafiti unaonesha kwamba asilimia kubwa ya wanaume wanaotumia gia hii kupata wanawake, si kweli kwamba wanatoka katika familia za aina hiyo. Hutumia kama njia tu, lakini baadaye hubainika kwamba walikuwa hawana uwezo kama waliosema awali. Athari inayoweza kupatikana kutokana ahadi hii ni pale ambapo unagundulika kuwa huna uwezo huo, lakini tayari mmeshazama mapenzini zaidi. Inawezekana awali wakati unaanzisha uhusiano naye, hukuwa katika kilele cha mapenzi sana.

Yawezekana ulimuona kama mwanamke wa kuzugia ndiyo maana ukatumia gia kubwa ili umpate, lakini baada ya kuwa naye kwa muda, ukagundua kwamba, kumbe moyo wako unampenda zaidi ya ulivyokuwa ukifikiria. Hili huwa kwa pande zote.

Kinachotokea hapa ni kwamba, wakati ukiwa umeshaamua kumpenda na kuwa naye, anagundua kwamba yupo na mwanaume muongo. Hata kama alikuwa anakupenda kwa kiwango gani, hawezi kukubali kuendelea na mwanaume wa aina yako.

NAFASI NZURI KAZINI

Wengine huwadanganya wenzi wao wanapokutana nao mara ya kwanza kuwa wana nafasi za juu katika sehemu zao za kazi. Wanaamini kwa kutumia gia hiyo, itakuwa rahisi zaidi kumpata mwanamke huyo. “Mimi kazini kwangu ni meneja, sishindwi kumnunulia gari. Ukiwa na mimi utafurahia maisha…kwanza una elimu gani? Nafikiria kukupachika sehemu ili uamini kuwa kweli mimi nakupenda sana…” Ahadi kama hii hutumika kwa baadhi ya wenzi wanapokutana mara ya kwanza.

Hata kama ni kweli wewe ni mkuu wa idara unayofanyia kazi ofisini kwako, si hoja muhimu inayohitajika kwa mwanamke unapokutana naye mara ya kwanza. Kwa mwenye uelewa atakudharau kwa kujikweza kwako, lakini mwingine anaweza kukubali si kwa sababu ya uongozi wako kazini, bali kwa mapenzi yake ya dhati kwako, lakini ndani ya moyo wake akiwa na malengo mengine.

Tayari ameshakuwa na imani kuwa atapata kazi akiwa katika uhusiano na wewe. Ataingia kwenye mapenzi akiwa anakupenda, lakini mtazamo wake juu yako utakuwa mwingine. Kwamba atakuwa anaishi na bosi. Ni kweli mapenzi si fedha, lakini inakuwaje pale unapomhakikishia mpenzi wako kuwa unazo, wakati unajua kuwa wewe ni hohehahe? Unataka nini hapo? Kuachwa?

PIMA AHADI ZAKO

Kikubwa rafiki zangu ninachotaka kuwaambia hapa ni vyema kupima kauli zako kabla ya kumwambia mwenzako. Usiahidi vitu ambavyo kamwe unajua kabisa huwezi kuvitimiza. Achana na mambo ya kizamani, mweleze mwenzako hali halisi ya maisha yako.

Kuwa huru, mapenzi si mali kama baadhi ya watu wanavyodhani. Kuwa wazi, naye atakuheshimu kutokana na ukweli wako. Kwa leo unaweza usione madhara ya kutoa ahadi hewa, lakini utakapokolea kwenye mapenzi, halafu ukashindwa kutimiza yale uliyokuwa unaahidi ndiyo mwanzo wa matatizo.

Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo.  Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

The post UNAIKUMBUKA AHADI YAKO WAKATI UNAANZISHA UHUSIANO?-2 appeared first on Global Publishers.



Comments

Popular posts from this blog

SHANGAZI NAE ANATAKA-07

join sugar mumy and dating whatsapp group link